Friday, February 23, 2007

Kinyang'anyiro cha Urais wa Marekani 2008, Obama kufurukuta?


Seneta Barack Husein Obama moja ya wanaotajwa kumrithi Bush akitangaza azma yake ya kuwania nafasi hiyo.
Ni uchaguzi unaovuta hisia si tu za wamarekani bali pia watu wa mataifa mbalimbali duniani kote. Kinadharia inaonekana kama vile Democratic watashinda uchaguzi huo kwa vile ndicho kinacholidhibiti baraza la Congress. Lakini pia suala la vita nchini Iraq limekipunguzia umaarufu chama cha Republican. Ndani ya Democratic kuna pilikapilika za kuwania kuteuliwa kwa ajili ya kukiwakilisha chama katika uchaguzi huo. Wanaotajwa sana ni Seneta Barack Obama na Hilary Clinton mke wa Bill Clinton. Je uraisi wa Marekani kuendelea kuwa mikononi mwa familia mbili yaani familia ya Bush na Clinton iwapo Hilary atapitishwa? Ni swali linalotokana na baadhi ya vikwazo anavyowekewa Barack Obama. Baadhi ya watu wanalifananisha jina la Obama kama Osama na pia Husein kama lile la Saddam. Wengine wanaenda mbali zaidi ya kwamba kwa vile yeye ni mweusi asitegemee kitu japo watu wanamkubali. Zaidi ya hayo Barack Obama anasemekana alipata kusoma nchini Afghanistan na kwa maana hiyo wanamuona kama mtu anayeweza kuimarisha urafiki kati ya Marekani na nchi za kiarabu. Kipyenga ndio hivyo kimelia na sisi yetu macho. Nani kumrithi Bush? Mweusi au mweupe? Tusubiri!!

Friday, February 16, 2007

Wataiva lakini kwa mwezi moja?

Mh. Waziri mkuu ndugu Edward Lowasa.

Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari imefanikiwa kuanzisha shule nyingi za sekondari. Jambo hilo halikwenda sanjari na maandalizi ya walimu. Ili kukidhi matakwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Magreth Sitta amebainisha kuwa zaidi ya walimu 9000 wanahitajika. Tayari walimu 3,124 waliohitimu (mwezi mmoja) kabla ya muda wao wataajiriwa moja kwa moja na serikali pamoja na wengine 250 waliokuwa wamestaafu watarejeshwa kazini. Nafasi 6,000 zitajazwa na waliomaliza kidato cha sita ambao watapigwa msasa wa mafunzo ya ualimu kwa muda wa mwezi moja. Mwombaji anatakiwa awe na alama mbili za kufaulu mtihani wa kidato cha sita na baada ya mwezi moja atakuwa mwalimu wa sekondari. Inahitajika miujiza itakayomfanya muhitimu wa kidato cha sita kuwa mwalimu bora kwa kipindi cha mwezi mmoja. Kimsingi kozi ya ualimu ina mambo mengi na inatakiwa isiwe pungufu ya miaka miwili. lngawa serikali inahitaji walimu wengi na kwa haraka, njia hii ina walakini kama kweli itatoa walimu bora au bora walimu.

Gari linapokwama kwenye tope la theluji!

Wakati tatizo kubwa katika nchi yetu ni barabara mbovu zinazosababisha magari kukwama, kwa wenzetu hali huwa tete katika msimu wa barafu. Barabara nyingi huwa zimefunikwa na tope la barafu kama inavyoonekana pichani. Huo ni mtaa wa Chuo kikuu cha New York.

Hakatizi mtu hapa!

Beki mahiri wa timu ya soka ya taifa (taifa stars), Shadrak Nsajigwa akiumiliki mpira mbele ya mchezaji wa Tigres du Brasil katika moja ya mechi za kujiandaa kabla ya kukabiliana na Senegal. Katika mechi hiyo Stars ilala kwa bao 1-0.

Saturday, February 10, 2007

Tunakuamkua Abraham Lincoln!


Tukiwa katika makumbusho ya Rais wa 16 wa Marekani Bw. Abraham Lincoln jijini Washington D.C.
George Washington (1789-1797) ndio mtu wa kwanza kula kiapo cha kuwa raisi wa Marekani akiongoza mlolongo wa watu 43. Miongoni mwa watu 43, kuna ambao kamwe hawatasahaulika kwa namna walivyoliongoza vyema taifa hilo lenye nguvu kubwa kiuchumi na kidola. Majina kama Abraham Lincoln (1861-1865), Theodore Roosevelt (1901-1909), John Kenedy (1961-1963) n.k ni miongoni mwa waliopata mafanikio makubwa katika nafasi hiyo ya uraisi. Kama ilivyo kwa msemo wa kiswahili "vizuri havidumu" Lincoln pamoja na kuwa kiongozi makini aliuwawa kwa kupigwa risasi na mtu aliyejulikana kwa jina la John Wilkes Booth. Hiyo ilikuwa Aprili, 14 1865 baada ya baadhi ya watu kutoridhishwa na sera zake za kuutokomeza ubaguzi na kuwatetea weusi ili kuleta usawa miongoni mwa raia aliokuwa akiwaongoza. Huyo ndio marehemu Lincoln, Raisi wa 16 wa Marekani 1861-1865.

Baada ya pindua pindua Dar, Bonde la ufa-RVF laitikisa Arusha.

"Imepimwa hii na kuthibitishwa na mganga kuwa haina RVF". Nahisi ndivyo asemavyo huyu muuzaji wa duka la nyama jijini Dar es Salaam.


Ni ugonjwa ambao huikumba mifugo hususan iliyo katika bonde la ufa na hii ndio sababu hasa ya kupewa jina hili. Binafsi natoka katika jamii ya wafugaji na ugonjwa ambao niliwahi kushuhudia madhara yake kwa binadamu ni kimeta. Nilishuhudia watoto wawili wa familia moja wakipoteza maisha na watu wengine watano wa familia hiyohiyo wakiponea chupuchupu kupoteza maisha kwa kula nyama ya ng'ombe aliyekuwa na kimeta. Kwa ujumla magonjwa haya ya mifugo aghalabu huwa mwiba na tishio siyo tu kwa maisha bali hata biashara. Kwa kawaida watu wengi katika kipindi hiki huwa wanakuwa makini katika kutumia mazao yatokanayo na mifugo. Lakini kuna wengine wachache ama kwa kutoelewa madhara yake au kwa kufanya makusudi hujikuta wakiathirika vibaya na kupoteza maisha kwa kuyatumia mazao ya mifugo athirika. Tayari serikali imeisha toa tamko kupitia mawaziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Prof. David Mwakyusa na yule wa Maendeleo ya Mifugo Mh. Anthony Diallo wakiwatahadharisha wananchi kuwa waangalifu wakati wa kula nyama na mazao yote yatokanayo na ng’ombe, mbuzi, nguruwe na kondoo. Ugonjwa huu wa bonde la ufa umejikita Arusha ukitokea nchini Kenya. Jambo la msingi hapa kujiuliza ni je huko vijijini ambako ndiko hasa kwenye wafugaji wengi kuna wataalamu wa mifugo wa kutosha na kama wapo wana vitendea kazi vya uhakika? Sijui maana kijijini kwangu mganga wa mifugo ni moja na anahudumia zaidi ya vijiji vitatu. Zemarcopolo nipo kwenye anga zako, tujadiliane.

Friday, February 9, 2007

Kama vile wanaimba "kama siyo juhudi zako Nyerere, CCM wangesoma wapiiii"


Wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu wakijumuika na wana-CCM wengine katika kusheherekea miaka 30 tangu kuzaliwa kwa chama hicho ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee.
Ni kama vile walijisahau na badala ya kusheherekea miaka 30 ya kuzaliwa kwa chama tawala (CCM), wanafunzi toka vyuo vya elimu ya juu walimtaka mwenyekiti wa chama taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano Mh. JK atoe msimamo wa serikali kuhusu wanafunzi wa taasisi hizo kuchangia 40% ya karo zao. Hakika majibu ya mheshimiwa Rais yalipokelewa kwa furaha pale aliposema serikali yake italiangalia upya suala hili. Kwa ujumla unapoongelea maendeleo ya taifa lolote hapa duniani ni nadra sana kutokuhusisha wasomi wa taifa hilo. Kimsingi wasomi kutoka taasisi za elimu ya juu ndio wataalamu wa kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuchochea maendeleo. Kwa ufupi 40% kwa mtanzania mwenye kipato cha chini ni mzigo usiobebeka na kama hivyo ndivyo na msimamo wa serikali ukabaki kama ulivyo kuna uwezekano mkubwa kwa vijana wengi kushindwa kuendelea na masomo ya juu. Hii maana yake ni kwamba tabaka kati ya walio nacho na wale wasio nacho litazidi kuongezeka huku maendeleo ya nchi kwa ujumla yakizidi kudidimia. Ni vema suala hili likaangaliwa upya kama alivyosema kiongozi wa nchi. Elimu kama chachu ya maendeleo haina budi kutolewa bila vikwazo.

Thursday, February 8, 2007

Heshima nyingine kubwa kwa nchi yetu.

Baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi Tanzania (JWTZ) wanaokwenda kulinda amani nchini Lebanon. Picha na Richard Mwaikenda.

Tanzania imepeleka jumla ya wanajeshi 80 wa Jeshi la Ulinzi Tanzania (JWTZ), kwenda nchini Lebanon kushiriki kulinda amani wakiwa ni sehemu ya vikosi vya Umoja wa Mataifa. Hii pia ni sifa nyingine kwa nchi yetu ikizingatiwa kuwa naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa (UN) pia anatoka Tanzania. Cha msingi ni kwamba askari hao ambao kati yao 11 ni wanawake, kuiwakilisha vyema nchi yetu kwa kuwa na nidhamu na kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu kama jeshi linavyoelekeza. Ama hakika hii itakuwa ni nafasi nzuri kuonyesha kwa vitendo yale waliyojifunza na pia kujifunza mengine watakayoyakuta huko kwenye operesheni ya kulinda amani. Mara ya mwisho Tanzania ilitoa askari wake kwenda kulinda amani katika mpango kama huo nchini Liberia kati ya mwaka 1993 na 1995. Mungu ibariki Tanzania na wanajeshi wetu huko Lebanon.

Wednesday, February 7, 2007

Kwa kasi hii Simba wa Teranga wajizatiti!!

Wachezaji wa timu ya soka ya Taifa (Taifa stars) al-maarufu kama "JK boys" wakiwa mazoezini katika kituo cha mafunzo ya michezo cha Fluminense jijini Rio de Janeiro Brazil. Kutoka shoto ni Mwaikimba, Nsajigwa, Maulid & Yusuf. Picha na Benny Kisaka.

Katika dunia hii hakuna lisilowezekana. Waingereza wana msemo wao "nothing imposible under the sun" wakimaanisha hakuna kisichowezekana hapa duniani. Kama hivi ndivyo, bila shaka hakuna kitakachoishinda timu ya taifa ya kabumbu kufanya kile kinachosubiriwa kwa shauku kubwa na mamilioni ya wapenda kandanda kote nchini. Ikiwa inaongoza katika kundi lake, maendeleo ya timu si mabaya na kwa muda wa mwezi moja itakuwa nchini Brazil kwa ajili ya kujifua kabla ya kucheza na Senegal moja ya nchi zilizopata mafanikio makubwa katika mchezo wa mpira wa miguu barani Afrika. Lakini hicho si kikwazo cha kuifanya timu yetu iwe imefungwa hata kabla ya mchezo. Chini ya mwalimu Maximo toka Brazil nchi ambayo kiwango chake katika mchezo huu ni cha hali ya juu, wachezaji wote wanayapokea mafunzo yake vizuri na wanajituma katika kufanya mazoezi kama inavyotakiwa na tena kwa moyo mkunjufu. Serikali ilitoa tamko ya kwamba haitavumilia vitendo vya utovu wa nidhamu katika kambi hiyo na pia ni jukumu la wachezaji wote kuwa na moyo wa uzalendo. Kwa ufupi ni kwamba mtanange kati ya Stars na Simba wa Teranga itajumuisha wanaume 22 kwa uwiano wa wachezaji 11 toka kila upande. Haogopwi mtu hapa! si Diof, Camara wala Diop. Ni mabao tu toka kwa Mwaikimba, Maulidi na Maftah. Mungu ibariki Stars, Mungu ibariki Tanzania.

Monday, February 5, 2007

Kiswahili nacho kilitumika kuwakilisha.

Waalimu andamizi wa lugha toka nchini Tanzania wakiwakilisha kwa kutumia lugha ya kiswahili katika kongamano la walimu mbalimbali wa lugha lililofanyika San Diego huko Califonia. Toka kushoto ni Mwl. Juma Binagirioba (Bowling Green University) na Mwl. Zablon Mgonja (Fisk University).
Lugha ni chombo muhimu cha mawasiliano. Kama zilivyo lugha nyingine, kiswahili kwa sasa kinazidi kupata umaarufu si Afrika tu bali hata nje ya Afrika kama vile Amerika na Ulaya. Mathalani vyuo vingi nchini Marekani vimeanzisha idara za kiswahili ambapo wanafunzi wengi wanajiandikisha kwa ajili ya kujifunza lugha hii. Kama ilivyo kwa mlima Kilimanjaro, pia wamarekani wengi wanaamini ya kwamba kiswahili sanifu kinazungumzwa nchini Kenya. Kutokana na imani hiyo hata walimu wengi wanaofundisha kiswahili katika vyuo hivyo wanatoka nchini Kenya. Pamoja na hayo walimu wachache toka Tanzania wamepata umaarufu mkubwa na ufanisi wa hali ya juu kwa muda mfupi walioutumia kufundisha. Kimsingi katika bara la Afrika kiswahili sanifu kinazungumzwa nchini Tanzania. Tatizo hapa ni kwamba kuna mapungufu katika kuitangaza Tanzania yetu, lugha yetu ya kiswahili pamoja na vivutio lukuki tulivyonavyo. Kuna msemo usemao "usipozungumza hautajulikana kama upo" . Kwa msemo huu ni muda muhali sasa kuitangaza nchi yetu.

Saturday, February 3, 2007

Tutaamka kikieleweka!!!

Ni kupumzika tu muda wowote na mahala popote. Picha kutoka darhotwire.

Ni wimbo ambao unatia fora karibu ulimwenguni kote. Wimbo wenyewe si mwingine bali ni ule uliopo kwenye albamu ya siku nyingi ya uchumi unaokwenda kwa jina la ajira. Kwa nchi zilizoendelea (za dunia ya kwanza) wimbo huu si maarufu sana. Kwa upande wa nchi zinazoendelea, wimbo huu ama hakika unatikisa vilivyo kila uchao. Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea inajitoa muhanga kwa kufanya kila linalowezekana kupunguza idadi ya wananchi hususani vijana wanaoimba kibao hiki japo kimepitwa na wakati ikizingatiwa ni karibu miaka 45 tokea nchi yetu ipate uhuru. Katika kufanikisha uwezeshaji kwa wananchi, serikali ya awamu ya nne chini ya Mh. Raisi J.Kikwete imeisha toa shilingi bilioni 1 kwa kila mkoa. Kwa ujumla ni mwanzo mzuri kama kutakuwa na usimamizi mzuri na masharti nafuu ili kuwawezesha walengwa haswaa kupatiwa mkopo huo. Vile vile ni wakati mzuri pia kwa benki zetu na asasi binafsi kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa wananchi ili kuchagiza mchakato mzima wa kuwawezesha wananchi kujiajiri wenyewe. Kama haya yote yatafanyika na mazingira mazuri yataandaliwa bila shaka hata waliolala wataamka. Namalizia kwa kusema "kama wao wameweza wana nini na sisi tushindwe tuna nini?"

Thursday, February 1, 2007

Rada, moto uliozimika na kulipuka tena.

Mh. JK Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akifafanua jambo kuhusu mustakabali wa Taifa letu.

Kwa kile kilichoelezwa kuwa ni harakati za kiusalama, serikali ya Tanzania mnamo mwaka 2002 ilitumia karibu Tshs bilioni 50 kwa ajili ya manunuzi ya Rada toka kwa serikali ya Uingereza kupitia shirika la BAE System. Mengi yalisemwa na watanzania wakati wa mchakato mzima wa suala la ununuzi wa rada na hatimaye yakasahaulika hadi mwaka huu baada ya wabunge wa Uingereza kuihoji serikali yao kwa kile kinachoonekana kuwa haikutenda haki kuiuzia Tanzania chombo hicho ambacho si cha kisasa tena kwa bei ya juu. Hivi sasa suala hilo kwa upande wa Uingereza limeachiwa Kitengo cha Kupambana na Makosa ya Ulaghai (SFO) ili kuchunguza madai kuwa kampuni ya BAE Systerm iliiuza rada hiyo kwa bei ya juu tofauti na bei halisi na pia kama ilitoa kamisheni ya sh. bilioni 12 kwa mtu aliyefanikisha ununuzi huo. Wakati hali ikiwa hivyo huko Uingereza, kwa upande wa Tanzania tayari yaliishafanyika maandamano kulaani ununuzi wa chombo hicho. Serikali imesisitiza kwamba inasubiri ripoti kutoka Uingereza ili kujua kama kuna watanzania waliohusika katika kashfa hiyo. Katika kulizungumzia sakata hilo serikali imesisitiza iwapo uchunguzi utabaini ya kwamba Tanzania ilidhulumiwa, kuna uwezekano mkubwa itatuma maombi kwa Serikali ya Uingereza ili kudai fedha zilizozidi. "Rada moto uliozimika na kulipuka upya".