Friday, March 2, 2007

Yangehifadhiwa kuliko kutapishwa!

Ama hakika Mungu mkubwa! Kutoka kupungua kwa kina cha maji hadi kutapishwa kwa maji katika bwawa la Mtera. Ashukuriwe kwa hilo. Ndio hivyo maji yamejaa pomoni na mamlaka husika imeamua kutapisha maji toka mabwawa ya Mtera na Kidatu. Hakuna atakayesahau uhaba wa umeme uliolikumba taifa mwaka jana. Chanzo cha tatizo kilikuwa ni kupungua kwa maji katika bwawa la Mtera. Leo bwawa limejaa kwa uwezo wake Allah, cha ajabu maji yanatapishwa badala ya kubuniwa njia mbadala za kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye endapo yatapungua. Baadhi ya nchi zina utaratibu wa kuhifadhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Mathalani Misri ipo Jangwani lakini kwa kutumia maji ya mto Nile wameweza kuhifadhi maji ya kutosha. Kwa maana hiyo hata mto Nile ukikauka hii leo, bado watu wa Misri watakuwa na uhakika wa kupata maji. Tanzania tungeiga mfano wa nchi ya Misri. Kimsingi hakuna sababu ya kumwaga maji yaliyozidi katika mabwawa ya Mtera na Kidatu na badala yake mamlaka husika zingebuni utaratibu wa kuyahifadhi maji hayo kwa ajili ya akiba ili siku zijazo ikitokea yamepungua iwe rahisi kuyatumia pasi kusubiri mvua. Tujifunze kupitia makosa kwani hatuna mkataba na Mungu kwamba mvua itakuwa ya kutosha kila mwaka.

Kuna ulazima wanja jipya kuzinduliwa na Real Madrid?


Pengine kusimama kwa uwanja mpya wa michezo ni miongoni mwa mambo yatayotufanya watanzania tusiisahau serikali ya awamu ya tatu. Tayari maandalizi ya ufunguzi wa kiwanja hicho cha michezo yanazidi kushika kasi. Real Madrid moja ya timu kubwa tena tajiri pengine kuliko vilabu vingine duniani imekubali kushiriki sherehe za uzinduzi wa uwanja huu kwa kutoa masharti magumu ikiwa ni pamoja na kupatiwa tiketi za ndege kwa ajili ya msafara wa watu 80 (round trip) kutoka Dar hadi Madrid-Hispania. Japo mwaliko huo ulitolewa na serikali na pia gharama zote zitalipwa na serikali bado hakukuwa na ulazima sana wa kujiingiza katika gharama kubwa kwa ajili ya timu moja (Real Madrid). Ingependeza kama zingealikwa timu za taifa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kama vile Togo, Nigeria, Afrika ya Kusini, Misri n.k. Hii ingetosha kabisa kuchagiza sherehe za ufunguzi wa uwanja mpya. Lakini pia ingekuwa ni manufaa makubwa katika kuijenga timu yetu ya taifa kimazoezi kwa kucheza na timu za taifa kutoka mataifa mbalimbali. Wewe unasemaje?

Chuo Kikuu cha New York kuwa na tawi Tanzania, chatengewa ekari 500!

Waziri wa Mali asili na utalii Prof. J4 Maghembe akiteta jambo na wadau wa Chuo kikuu cha New York ikiwa ni jitihada za serikali ya awamu ya nne kuitangaza Tanzania na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini. Wadau wa Chuo kikuu cha New York wameonyesha dhamira ya kufungua tawi la chuo hicho nchini Tanzania. Serikali imekipatia chuo hicho ekari 500 kwa ajili ya kufungua tawi hilo ambalo litaitwa NYU in Tanzania. Akiwa chuoni hapo Waziri wa mali asili na utalii aliwahakikishia uwepo wa eneo hilo. Hiyo ilikuwa tarehe 22/2/ 07. Chuo kikuu cha New York tayari kina matawi nchini Brazil, Canada,Uingereza na Ghana. Huenda Tanzania ikaingia kwenye hiyo orodha.