Friday, March 2, 2007

Kuna ulazima wanja jipya kuzinduliwa na Real Madrid?


Pengine kusimama kwa uwanja mpya wa michezo ni miongoni mwa mambo yatayotufanya watanzania tusiisahau serikali ya awamu ya tatu. Tayari maandalizi ya ufunguzi wa kiwanja hicho cha michezo yanazidi kushika kasi. Real Madrid moja ya timu kubwa tena tajiri pengine kuliko vilabu vingine duniani imekubali kushiriki sherehe za uzinduzi wa uwanja huu kwa kutoa masharti magumu ikiwa ni pamoja na kupatiwa tiketi za ndege kwa ajili ya msafara wa watu 80 (round trip) kutoka Dar hadi Madrid-Hispania. Japo mwaliko huo ulitolewa na serikali na pia gharama zote zitalipwa na serikali bado hakukuwa na ulazima sana wa kujiingiza katika gharama kubwa kwa ajili ya timu moja (Real Madrid). Ingependeza kama zingealikwa timu za taifa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kama vile Togo, Nigeria, Afrika ya Kusini, Misri n.k. Hii ingetosha kabisa kuchagiza sherehe za ufunguzi wa uwanja mpya. Lakini pia ingekuwa ni manufaa makubwa katika kuijenga timu yetu ya taifa kimazoezi kwa kucheza na timu za taifa kutoka mataifa mbalimbali. Wewe unasemaje?

7 comments:

Anonymous said...

Mtanzania!
Hiyo itakuwa fursa nzuri kwa nchi yetu kujulikana miongoni mwa mataifa tajiri duniani. Kumbuka soka ni biashara and if that is the case there is a need to advertise.
Thank you. Your blogspot is good.

Anonymous said...

Mtanzania,

Mi nachokoza tu. Mosi, hivi hiki si kiini macho. Akufukuzaye hakwambii toka. Inawezekana kabisa Real Madrid hawataki kuja huku. Wakaona kuwa wakitukatalia moja kwa moja na Mheshimiwa wetu JK alikuwa kwao miezi ya karibuni basi itatuumiza sana. Hivyo, wakaona watupe masharti magumu ambayo kwa kupima harakaharaka tu Watanzania wangesema tumeshindwa sisi. Maana hiyo gharama yake, nasikia ni aghali kwelikweli. Ambapo fedha hizo tungewekeza katika kuitangaza Tanzania kwa njia nyingine basi tungegusa kila kitu kilichopo TZ. Hivyo, mimi nahisi hawa jamaa walitutolea nje kiungwana, hebu tulione hilo.
Pili, hivi suala hili lina tofauti sana na mgogoro wa rada? Maana yake, tunahitaji kuingia gharama kubwa kiasi hiki kwa ajili ya tukio hilo? Je, ni kweli litalipa kama wanavyodai baadhi ya watetezi? Je, utangazaji huo wa nchi katika muda mfupi utadumu kwa miaka mingapi?
Hivi, nusu ya fedha hizo si zingepelekwa kule Rukwa ambako hivi sasa hakufikiki na maisha ya watu yako hatarini kwa kukosa mawasiliano ya barabara?
Where are our priorities?

Anonymous said...

Deosimba!
Ndio hivyo imeishatangazwa kwamba kuja kwa Real ni lazima!

Jeff Msangi said...

Mtanzania,
Mimi nadhani kutumia mabilioni ya fedha kuialika sio tu Real Madrid bali timu yoyote duniani kwa kisingizio cha "kuitangaza nchi" au "biashara" ni kosa.Au niseme mojawapo ya makosa mengi ya kiuongozi,maamuzi na utawala ya nchi yetu.

Inaeleweka kwamba soka ni mchezo unaopendwa sana barani Afrika na duniani kote.Lakini mapenzi hayo yasiingiliane na maisha halisi ya mtanzania.Tanzania bado inabakia kuwa nchi changa na wengi ya wananchi wake wanaishi maisha duni kabisa.Yapo masuala mengi sana ambayo ni lazima tuyape kipaumbele kabla ya michezo hususani ambayo itaigharimu nchi mabilioni ya shilingi.

Simon Kitururu said...

Kwa mtazamo wangu haikulazimika kabisa kuzindua uwanja kwa staili hii.

Anonymous said...

Safi sanaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa hii ni fahari yetu

Anonymous said...

Wazo la kuwa uzinduzi ungejumuisha timu mbalimbali na majirani zetu ni wazo la mwananchi mwenye kujali nchi na mali yake. Ila wale wanaojali ufahari wanaona kuwa tunahitaji Real Madrid.

Kama kuna shule iliyoko kilometa kadhaa toka ikulu ambayo haina maabara na vifaa vingine muhimu, inakuwaje hakuna fedha za kujenga maabara kwa ajili ya wanasayansi wa kesho ila fedha za kuleta Madrid? Kama unataka kuwaona Madrid kanunue televisheni. Tunaongelea nchi ambayo haijui inakwenda wapi. Inakwendakwenda tu, kisha tunaletewa Real Madrid kama kidonge cha kutulevya. Mtaani watu wataanza ushabiki, "aisee, Kikwete kiboko katuletea Madrid." Halafu anayesema hivyo anapomaliza, anatazama huku na kule kutafuta mtu wa kumuomba hela ya nauli.