Friday, March 2, 2007

Yangehifadhiwa kuliko kutapishwa!

Ama hakika Mungu mkubwa! Kutoka kupungua kwa kina cha maji hadi kutapishwa kwa maji katika bwawa la Mtera. Ashukuriwe kwa hilo. Ndio hivyo maji yamejaa pomoni na mamlaka husika imeamua kutapisha maji toka mabwawa ya Mtera na Kidatu. Hakuna atakayesahau uhaba wa umeme uliolikumba taifa mwaka jana. Chanzo cha tatizo kilikuwa ni kupungua kwa maji katika bwawa la Mtera. Leo bwawa limejaa kwa uwezo wake Allah, cha ajabu maji yanatapishwa badala ya kubuniwa njia mbadala za kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye endapo yatapungua. Baadhi ya nchi zina utaratibu wa kuhifadhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Mathalani Misri ipo Jangwani lakini kwa kutumia maji ya mto Nile wameweza kuhifadhi maji ya kutosha. Kwa maana hiyo hata mto Nile ukikauka hii leo, bado watu wa Misri watakuwa na uhakika wa kupata maji. Tanzania tungeiga mfano wa nchi ya Misri. Kimsingi hakuna sababu ya kumwaga maji yaliyozidi katika mabwawa ya Mtera na Kidatu na badala yake mamlaka husika zingebuni utaratibu wa kuyahifadhi maji hayo kwa ajili ya akiba ili siku zijazo ikitokea yamepungua iwe rahisi kuyatumia pasi kusubiri mvua. Tujifunze kupitia makosa kwani hatuna mkataba na Mungu kwamba mvua itakuwa ya kutosha kila mwaka.

2 comments:

Anonymous said...

Ni jambo zuri lakini tatizo ni kwamba teknolojia yetu ipo chini kiasi kwamba si rahisi kufanikiwa kujenga mabwawa ya kutunza maji.

Simon Kitururu said...

Naamini niuamuzi tu. Ni mambo ya kujua nini muhimu. Naamini kwamba maswala ya umeme ni kwamba serikali haijaipa kipaumbele tu. Halafu na uhakika ndani ya mwaka, mgao wa umeme utarudi. Kuna mambo mengine tunamsingizia Allah wakati hayamuhusu. Yeye kashatupa akili na inatosha kwa hilo. Kuna mambo tumlalamikie na kuomba kisawasawa. Lakini kuna mengine nahisi ni aibu hata kumhusisha.Na katika mambo ya aibu kumhusisha, moja wapo ni umeme Tanzania.