Saturday, April 28, 2007

Kitu hicho!

Ama hakika Teknolojia inakua kila uchao! Hiki kifaa sijui kinaendaje. Wasiwasi wangu ni pale tu kitakapokwaruzwa kama si kugongwa. "weekend njema".

Inawezakana matunda yameanza!


Ziara ya Shaikh Saud bin Saqral Al Qasimi ambaye ni Naibu mtawala wa Ras al Khaiman inaweza ikafungua milango ktk suala zima la uwekezaji hapa nchini Tanzania. Ras Al Khaiman ni miongoni mwa nchi 7 zinazounda muungano wa EMIRATES. Kiuchumi jumuiya ya EMIRATES wamepiga hatua. Ni vema basi viongozi wetu wajifunze mengi toka kwa kiongozi huyo ili kuinua na hatimaye kukuza uchumi wa nchi yetu. Pengine ziara hii ni mojawapo ya matunda ya ziara za viongozi.

Wednesday, April 25, 2007

Hongera Tanzania kwa kutimiza miaka 43 ya Muungano!

Kila la kheri ktk kusheherekea sikukuu ya Muungano.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tz, Mh JK ni kama vile anamwambia Rais wa Burkina Faso "Muungano wetu hautatetereka, nitaulinda na kuutunza kwa kuuimarisha zaidi"

Wednesday, April 18, 2007

Hivi ulifanyalo ndo hasa ulistahili kulifanya!!!


Pichani baba watoto akiwa makini kutoa maelekezo kwa wanawe wanaojaribu kuchora huku mama yao akitazama. Ni njia thabiti ya kuendeleza vipaji.

Kipaji (ability/talent) ni ile hali ambayo kiasili mtu anakuwa na uwezo au mapenzi ya kufanya jambo fulani. Aghalabu vipaji huonekana tangia utotoni. Kila mtoto huwa anaonyesha kile anachokipenda (interest) kwa kujaribu kukifanya mara kwa mara. Kawaida vipaji vinapaswa kuendelezwa na kukuzwa katika mazingira mazuri. Wawajibikaji wakuu kwa hilo ni wazazi au walezi (care givers). Kwa kufanya hivyo watoto watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuyafanya yale wayapendayo. Kama mtoto anaonyesha mapenzi katika kusakata kabumbu basi ni vema aipate elimu yake katika shule zenye mchepuo wa michezo. Sina uhakika kama hili nilifanyalo ndio hasa nililokuwa nikilipenda tangu utotoni. (sikufuru). Lakini nakumbuka nilikuwa napenda sana kuwa muuza duka na nilikuwa nikiwasumbua sana wazazi wangu kwa hilo. Kwa undani huenda kipaji changu kilikuwa biashara. Katika nchi zilizoendelea suala hili linazingatiwa sana kwa ushirikiano wa wazazi na serikali. Kwa kuhitimisha, napenda nikuulize swali dogo mpenzi msomaji, Je hiyo shughuli yako uifanyayo au hiyo kozi unayosoma ni ile hasa ambayo inaendana na kipaji chako?

Tuesday, April 10, 2007

Bifu sasa limekwisha, "sisi wamoja na tuchape kazi".

Pichani "tusameheane mzee kwa yaliyotokea" Kutoka kushoto ni Mh. Spika Sitta , Mh. W/M Lowasa na Mh. Malima. (Picha na Hilary Bujiku)
Siasa bwana ina mambo yake! Mikwara miiiiingi! Binafsi sikuona sababu ya kulumbana sana na kutumia fedha zilizotumika kwa hoja ya Mh. Malima kuhusu muda unaotolewa na ITV kwa viongozi wa kitaifa dhidi ya ule anaopewa Mwenyekiti mtendaji wa IPP katika taarifa za habari za ITV. Hili lilitokea kikao cha bunge kilichopita. Nafikiri kulikuwa na bado kuna hoja nyingine nzito na nyeti zaidi ya hiyo ambazo zilistahili na bado zinastahili mjadala.

Monday, April 9, 2007

Pozi lake lina mvuto!

Moja ya hazina kubwa ya taifa. Anaonekana kama anasema "ok. nipo tayari nipige picha". Pundamilia huyu ni moja ya vivutio vingi vilivyo katika hifadhi ya taifa ya Ngorongoro Crater. Katika karne hii ya sayansi na teknolojia ni muhimu kuvitangaza vivutio hivi. Kama ilivyo habari, biashara pia ni kutangaziana!

Waweza usiamini, ila ndo ukweli!

Pichani ni makazi ya watu katika mji wa Nashville-TN. Picha nyingi kutoka nchi zilizoendelea huwa ni za kuonyesha mazuri il-hali kutoka Afrika ni za kuonyesha mabaya. Anyway, ninachotaka kukiwakilisha hapa ni kwamba si kila kitu ni shwari katika nchi zilizoendelea kama hii picha ya makazi ya watu katika mji wa Nashville-U.S inavyothibitisha.

Sunday, April 8, 2007

Yupi bora, Raisi mzee au kijana?

Raisi Abdulwaye Wade wa Senegal. Staili yake ya kunyoa ni ya kipekee miongoni mwa viongozi wa juu.

Friday, April 6, 2007

Maadhimisho ya mauaji ya mwaka 1994 nchini Rwanda.




Mauaji yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 kamwe hayatasahaulika. Si kwa wanyarwanda tu bali hata kwa wapenda amani kote duniani ingawa leo ni miaka 13 tangu yalipotokea. Sababu kubwa ya mauaji ilikuwa ni tofauti za ukabila baina ya makabila makuu mawili yaani wahutu na watutsi. Wengi wa waliouwawa walikuwa ni watutsi na wahutu wachache. Zaidi ya watu 800,000 walipoteza maisha na miongoni mwao 500,000 walikuwa watutsi. (Pia inakadiriwa waliokufa walikuwa zaidi ya 1,000,000). Mauaji haya yalifanywa na vikundi vya wanamgambo wa Kihutu maarufu kama Interahamwe na Impuzamugambi. Zilikuwa takribani siku 100 za umwagikaji wa damu usio na mfano kuanzia April 6 mpaka katikati ya mwezi wa saba. Lakini katika kuadhimisha siku hii hatuna budi kuungana na wenzetu wa Rwanda katika kudumisha udugu,mshikamano na umoja bila kujali tofauti za ukabila,udini na za kisiasa kwani tofauti katika nyanja hizi aghalabu ndio chanzo cha mifarakano miongoni mwa wanajamii. Hongera serikali ya Rwanda kwa mwanzo mzuri wa kuijenga Rwanda mpya yenye uchumi unaokua, miundo mbinu bora na pia huduma bora za kijamii.

Wednesday, April 4, 2007

Nyota yake iling'ara tokea akiwa bado kinda.

Vipaji (talents) mara nyingi huonekana tokea utotoni. Franco akiwa na miaka 7 alifanikiwa kutengeneza gitaa kwa kutumia lililokuwa kopo la bati la kuhifadhia mafuta ya kupikia. Alilitumia gitaa hilo kutoa burudani kwenye mechi za kandanda. Alifanikiwa kupata gitaa halisi alipokuwa na umri wa miaka 11. Wakati huo alikuwa kama mpiga gitaa wa muda tu katika studio ya Loningisa iliyokuwa ikimilikiwa na Wagiriki huko nchini Zaire. Kipindi hicho, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa chini ya utawala wa Ubelgiji. Mwaka 1956, Makiadi alifanikiwa rasmi kuanzisha bendi ya OK Jazz ambayo baadaye ilikuja kujulikana kama TPOK Jazz. Aliongeza "TP=Tout Puissant" yenye maana ya "wote wana nguvu". Tizama moja ya kazi zake hapa.

Alipata kuitwa "Baba wa muziki wa Afrika". Ni Franco Luambo Makiadi!

Franco Makiadi alipata kuitwa baba wa muziki wa Afrika. Serikali ya Zaire ilimtunuku heshima ya "Grande MaƮtre", heshima ambayo ilikuwa mahsusi kwa majaji na wasomi. Pamoja na hayo, Franco aliwahi kufungwa na pia kuzuiliwa kutoka nje ya nchi kwa sababu ya ujumbe uliokuwa kwenye baadhi ya nyimbo zake. Baada ya kuondolewa kizuizi, Luambo Makiadi alipata kufanya ziara ya kimuziki nchini Uingereza na Marekani katikati ya miaka ya 80.

Luambo Makiadi aliimba kwa kutumia lugha ya Lingala na ujumbe katika nyimbo zake ulihusu mambo ya kijamii. Staili yake ya kufikisha ujumbe ni ya kutumia mafumbo huku ikichagizwa na maelezo ya hapa na pale. Aghalabu, ujumbe katika nyimbo zake huwa umefichama. Alipata kuimba juu ya serikali, nasibu mbalimbali za maisha mathalani ugomvi kati ya wanandoa. Binafsi aliipenda kazi yake na kibao alichokipenda na kilichopata kuitikisa Africa na kumletea heshima kubwa ni "Mario". Kibao hiki kinaelezea mapenzi baina ya kijana msomi lakini mvivu (hohehahe) na mwanamama mtu mzima mwenye uhakika wa maisha. Hatimaye kijana alifukuzwa na mwanamama huyo kwa kuonekana ni mnyonyaji (mchunaji). Ama hakika kibao hiki kilitia fora ya mauzo na bado kinazidi kuuzika hadi hii leo.
Lwambo Makiadi alifariki mwaka 1989 na mazishi yake yalifanywa kuwa ya kiserikali na alipewa heshima zote za kitaifa chini ya Serikali ya Zaire enzi hizo Raisi akiwa hayati Mobutu Seseseko "Kuku wa Zebanga". Viongozi na wawakilishi mbalimbali wa kitaifa kutoka nchi za Kiafrika na Wazaire mamia kwa maelfu walijumuika jijini Kinshasa kutoa heshima zao za mwisho kwa Franco.Serikali ilitangaza mapumziko ya siku 4 na stesheni zote za redio zilikuwa zikiporomosha muziki wa Franco mchana kutwa na usiku kucha. Huyo ndiye hayati Franco Luambo Luazo Makiadi. Matunda yake ni mwanamuziki Madilu Multi System. Daima utakumbukwa.
R.I.P Franco Makiadi.

Tuesday, April 3, 2007

Kama vile ice-cream za Bakhresa!

Biashara ya kuuza barafu (ice-cream) ni maarufu sana katika jiji la Dar-es-Salaam. Pichani ni biashara kama hiyo katika jiji la New York. Kwa ujumla mazingira ya biashara hii jijini NY yanafanana kabisa na yale ya jijini Dar-es-Salaam.