Wednesday, April 4, 2007

Alipata kuitwa "Baba wa muziki wa Afrika". Ni Franco Luambo Makiadi!

Franco Makiadi alipata kuitwa baba wa muziki wa Afrika. Serikali ya Zaire ilimtunuku heshima ya "Grande Maître", heshima ambayo ilikuwa mahsusi kwa majaji na wasomi. Pamoja na hayo, Franco aliwahi kufungwa na pia kuzuiliwa kutoka nje ya nchi kwa sababu ya ujumbe uliokuwa kwenye baadhi ya nyimbo zake. Baada ya kuondolewa kizuizi, Luambo Makiadi alipata kufanya ziara ya kimuziki nchini Uingereza na Marekani katikati ya miaka ya 80.

Luambo Makiadi aliimba kwa kutumia lugha ya Lingala na ujumbe katika nyimbo zake ulihusu mambo ya kijamii. Staili yake ya kufikisha ujumbe ni ya kutumia mafumbo huku ikichagizwa na maelezo ya hapa na pale. Aghalabu, ujumbe katika nyimbo zake huwa umefichama. Alipata kuimba juu ya serikali, nasibu mbalimbali za maisha mathalani ugomvi kati ya wanandoa. Binafsi aliipenda kazi yake na kibao alichokipenda na kilichopata kuitikisa Africa na kumletea heshima kubwa ni "Mario". Kibao hiki kinaelezea mapenzi baina ya kijana msomi lakini mvivu (hohehahe) na mwanamama mtu mzima mwenye uhakika wa maisha. Hatimaye kijana alifukuzwa na mwanamama huyo kwa kuonekana ni mnyonyaji (mchunaji). Ama hakika kibao hiki kilitia fora ya mauzo na bado kinazidi kuuzika hadi hii leo.
Lwambo Makiadi alifariki mwaka 1989 na mazishi yake yalifanywa kuwa ya kiserikali na alipewa heshima zote za kitaifa chini ya Serikali ya Zaire enzi hizo Raisi akiwa hayati Mobutu Seseseko "Kuku wa Zebanga". Viongozi na wawakilishi mbalimbali wa kitaifa kutoka nchi za Kiafrika na Wazaire mamia kwa maelfu walijumuika jijini Kinshasa kutoa heshima zao za mwisho kwa Franco.Serikali ilitangaza mapumziko ya siku 4 na stesheni zote za redio zilikuwa zikiporomosha muziki wa Franco mchana kutwa na usiku kucha. Huyo ndiye hayati Franco Luambo Luazo Makiadi. Matunda yake ni mwanamuziki Madilu Multi System. Daima utakumbukwa.
R.I.P Franco Makiadi.

1 comment:

Anonymous said...

Kumbe Franco alikubalika sana. Nimefurahishwa na namna serikali ya Zaire ilivyompatia heshima kubwa hata baada ya kufariki.