Friday, April 6, 2007

Maadhimisho ya mauaji ya mwaka 1994 nchini Rwanda.




Mauaji yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 kamwe hayatasahaulika. Si kwa wanyarwanda tu bali hata kwa wapenda amani kote duniani ingawa leo ni miaka 13 tangu yalipotokea. Sababu kubwa ya mauaji ilikuwa ni tofauti za ukabila baina ya makabila makuu mawili yaani wahutu na watutsi. Wengi wa waliouwawa walikuwa ni watutsi na wahutu wachache. Zaidi ya watu 800,000 walipoteza maisha na miongoni mwao 500,000 walikuwa watutsi. (Pia inakadiriwa waliokufa walikuwa zaidi ya 1,000,000). Mauaji haya yalifanywa na vikundi vya wanamgambo wa Kihutu maarufu kama Interahamwe na Impuzamugambi. Zilikuwa takribani siku 100 za umwagikaji wa damu usio na mfano kuanzia April 6 mpaka katikati ya mwezi wa saba. Lakini katika kuadhimisha siku hii hatuna budi kuungana na wenzetu wa Rwanda katika kudumisha udugu,mshikamano na umoja bila kujali tofauti za ukabila,udini na za kisiasa kwani tofauti katika nyanja hizi aghalabu ndio chanzo cha mifarakano miongoni mwa wanajamii. Hongera serikali ya Rwanda kwa mwanzo mzuri wa kuijenga Rwanda mpya yenye uchumi unaokua, miundo mbinu bora na pia huduma bora za kijamii.

2 comments:

Simon Kitururu said...

Nasikia kuanzia Raisi mpaka watu kadhaa wa kadhaa wanampiga vita Paul Rusesabagina, ambaye maandishi yake yalizaa sinema ya Hotel Rwanda. Yeye anadai anahisi mauaji haya yatajirudia. Hicho ndio kisa cha kupigwa vita yeye. Lakini tuombee mambo kama haya yasitokee tena

MTANZANIA. said...

Kitururu!
Hizo habari ni nzito. Lakini si za kupuuza hata kidogo. Nilibahatika kufanya mazungumzo mafupi na balozi wa Rwanda ktk UN Prof. Nsezimana na alisema kuwa mauaji ya 1994 yalitabiriwa tokea mwaka 1959. Kwa maana hiyo bwana Paul asitengwe ila asikilizwe.