Tuesday, January 30, 2007

Ni shule mtindo mmoja bila kujali umekalia kiti au umekaa chini.

Hali inavyokuwa wakati wa muhadhara katika moja ya kumbi za mihadhara chuo kikuu Mlimani.

Chuo kikuu cha Dar es Salaam pengine ndio taasisi kubwa ya elimu ya juu kuliko taasisi nyingine zote. Si tu ni taasisi kubwa kwa kuwa na muda mrefu tokea kuanzishwa, bali pia ndiyo taasisi pekee inayodahiri idadi kubwa ya wanafunzi kwa ajili ya stashahada, shahada, na shahada za uzamili. Taasisi hii kwa sasa inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwa ni pamoja na uwiano usiokuwa sawia baina ya idadi ya wanafunzi na vitendea kazi kwa ujumla wake. Mathalani kumbi za mihadhara zilizojengwa kwa ajili ya kupokea wanafunzi 400, kwa sasa zinalazimika kutumiwa na wanafunzi zaidi ya 1000. Katika nadharia ya kweli ili mwanafunzi aelewe vizuri kile anachofunzwa anapaswa kuwa katika mazingira mazuri huku akili ikiwa imetulia. Lakini kwa chuo chetu hiki hali ni tofauti maana muda mwingi mwanafunzi anawaza kama kipindi kijacho utapata kiti au utaketi chini tena. Ndio hivyo kwa mazingira hayo hayo watu wanahitimu kila mwaka. Ni wakati sasa kwa uongozi wa chuo kwa kushirikiana na serikali yetu kuyabadili mazingira ya chuo ili kiwe na hadhi ya chuo kikuu. "Elimu ndio ufunguo wa maendeleo".



Vivutio si kwa ajili ya wageni tu, hata wazalendo tunaweza kuwa watalii.

(Pichani watanzania waishio Moshi walioamua kutembelea vivutio mbalimbali kama bango linavyojionyesha. Picha kwa hisani ya Juma Iddi Issa -wa kwanza toka kushoto.)

Tanzania yetu imejaliwa kuwa na vivutio vingi kama vile mbuga za wanyama, mabonde mazuri ya kuvutia, mlima mrefu wa Kilimanjaro, maziwa na mito mingi karibu kila kona ya nchi. Lakini wageni toka nje ya nchi ndio kwa asilimia kubwa wanaovitembelea vivutio hivyo ikilinganishwa na wazawa. Binafsi naweza sema ni kasumba ambayo wazalendo tumejijengea ya kwamba vivutio hivi ni kwa ajili ya wageni (watalii). Kimsingi si wanaotoka nje tu ndio wanapaswa kuwa watalii bali hata sisi watanzania tunaweza kabisa kuwa watalii kwenye vivutio mbalimbali ndani ya nchi yetu. Cha msingi hapa ni serikali kupunguza viingilio kwa wazawa ili kutoa nafasi kubwa kwa wananchi bila kujali vipato vyao. Ni aibu mtu kutoka Amerika ya kusini au Mashariki ya mbali na kuuetembelea mlima Kilimanjaro ili hali mimi na wewe tuliozaliwa na kukulia Tanzania si tu hatujawahi kuutembelea bali hata historia yake hatuijui vizuri. "Nakupenda Tanzania"

Sunday, January 28, 2007

Uzalendo upewe kipaumbele badala ya unazi!

Wawakilishi wa Tanzania ktk ligi ya mabingwa Afrika-Yanga kabla ya ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya AJSM ya Comoro. (Picha kwa hisani ya Muhidin Michuzi)
Moja ya sera za serikali ya awamu ya nne chini ya Mh. JK ni kuinua michezo na kwa kuanza mchezo wa mpira wa miguu maarufu kama kandanda ndio umepewa kipaumbele.Kutambulika kwa nchi yetu katika ramani ya kabumbu barani Afrika na ulimwenguni kwa ujumla kutatokana na kuimarika kwa vilabu vyetu.Ili kuwa na timu nzuri ya taifa ni vizuri tukawa na vilabu bora vyenye kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Kwa ujumla Yanga na Simba ndio vilabu vikubwa katika soka nchini Tanzania vinavyovuta hisia za mashabiki lukuki. Kuwa mnazi wa Simba au Yanga ni utashi lakini ni vema jambo hili likaenda sanjari na uzalendo unapofika wakati wa mechi za kimataifa. Mathalani mwaka huu Yanga ndio wawakilishi wa nchi yetu katika ligi ya mabingwa Afrika ili-hali Simba ni wawakilishi katika kombe la CUF. Kimsingi umefika wakati sasa kwa mashabiki wa timu za Yanga na Simba kuuvaa uzalendo na kuondoa tofauti za kiushabiki wakati moja ya timu zetu inapokuwa inaliwakilisha taifa letu. Mechi za uwanja wa nyumbani ni mechi muhimu ambazo ni vizuri timu zetu zikazitumia kuvuna ushindi mnono.Kisaikolojia mashabiki wana nafasi yao katika kufanikisha au kuzorotesha ushindi ama kwa kushangilia au kwa kuzomea.Si vema na wala si busara kwa watazamaji wanaoingia uwanja wa taifa kutowashangilia wawakilishi wetu kwa kisingizio cha unazi wa Yanga na Simba. Kwa ujumla timu zetu za Yanga na Simba zina nia na uwezo wa kulitoa kimasomaso taifa letu katika mechi za kimataifa.Wanazi tutoe ushirikiano wa kutosha. Mungu Ibariki Tanzania.

Saturday, January 27, 2007

Nembo za taifa kielelezo cha uzalendo,sheria iruhusu zitumike.


Ama hakika rangi za bendera yetu zinapendeza.
Bendera ni miongoni mwa nembo za taifa na pia ni kitu cha kujivunia kwa kila mwananchi. Kimsingi bendera ni alama ya utaifa na pia ni kielelezo halisi cha uzalendo.Umefika wakati sasa iwe ni ruhusa kwa wananchi kuitumia bendera ya taifa kwani bendera ya taifa ya nchi ndio utambulisho wa nchi na kwa mtu yeyote mzalendo anapoiona bendera ya taifa lake ikipepea mahali fulani, hupata mvuto wa kipekee na pia hukumbuka nyumbani.Mathalani kipindi hiki cha kuinua kandanda Tanzania ni vema ikawa ni ruhusa kwa rangi za bendera kutumiwa na watanzania katika kuishangilia timu ya taifa ya soka na hata timu za taifa za michezo mingine.Vile vile iwe ruhusa kwa watanzania kushona na kununua nguo zenye rangi ya bendera ya taifa tofauti na sasa ambapo watanzania tunabanwa na sheria ya nchi.Mathalani katika mataifa kama Uingereza au Marekani, ni rahisi kukuta nguo, kofia, kalamu, vitambaa na hata makaratasi yenye rangi zinazoonyesha bandera ya nchi hizo yakiwa yamepamba mitaa ya miji. Ni muda muafaka kwa sheria za nchi yetu kufanyiwa marekebisho.Vinginevyo nchi yetu itaendelea kutotambulika na hali kadhalika sifa kemkem za nchi yetu kama vifutio vya utalii vitaendelea kutangazwa kuwa vipo nchini Kenya na wala si Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.

Friday, January 26, 2007

Ukitembea utaona au kusikia mengi.

Pichani mwanadada akila pozi na mbwa wake.
Walipata kunena wahenga "ukishangaa ya Musa utayaona ya Firauni". Hawakuishia hapo pia waliibuka na msemo mwingine "tembea uone". Kwa ujumla hizi semi mbili zina maana kubwa iliyofichamana. Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini Tanzania ana kibwagizo fulani cha "mbado".Niliwauliza maswali machache marafiki zangu waliopo Tanga na majibu yao yalikuwa mbado. Maswali yangu yalikuwa kama hivi:-
Mimi- Mmewahi kuona mbwa akipigwa busu?
Wao-mbado.
Mimi- Mmewahi kusikia mbwa akiitwa "he" au "she"?
Wao-mbado.
Mimi-mmewahi kusikia mbwa akilala chumba achilia mbali kitanda kimoja na binadamu?
Wao-mbado.
Mimi- jamani hamjayaona wala kuyasikia hayo yote?
Wao-mshangao!!-mbado.
Ndio hivyo hayo mambo yapo.Baada ya kutembea nilibahatika kujua kwamba hayo yote niya kawaida katika jamii za kimagharibi. Mathalani hapa Marekani mbwa hana nafasi kubwa katika suala zima la ulinzi bali ni rafiki mkubwa wa binadamu hali inayopelekea mnyama huyo apewe heshima kubwa na upendo wa hali ya juu. Kupigwa busu, kupewa heshima ya ubinadamu na hata kushea sehemu za kulala ni mambo ya kawaida anayofanyiwa mnyama huyu hapa Marekani. Baada ya kufanya udadisi wa hapa na pale kwa wenyeji wangu wa hapa, majibu niliyopata ni kwamba mnyama mbwa ni rafiki yao mkubwa kwa misingi ya kwamba huwa anawaondolea upweke wale wenye upweke na pia hutoa kampani kwa wasio kuwa na kampani. Bado kwangu imekuwa ngumu kuwaelewa wenzetu hawa na huu urafiki wao kwa hawa wanyama. Uchunguzi wangu usiokuwa rasmi sana unaonyesha wanaume wengi wanakuwa pamoja na mbwa jike na hali kadhalika wanawake wengi wana midume ya mbwa. Nimeiweka hii mada ili nipate maoni kutoka kwa yeyote anayejua lolote juu ya hili suala.

Tuesday, January 23, 2007

Kama ni koleo, basi liitwe koleo.

(Pichani mwenye batiki ni mke wa mwanaharakati mahiri kutoka Kenya aitwaye Ngugi wa Thiong'o. Wengine ni wanafunzi wa NYU kutoka nchini Tanzania na Kenya.)
Kwa umri nilionao nimepata kuyasikia maneno mbalimbali yakiwa na maana tofauti.Mengi ya maneno yasiyotamkika mbele ya hadhira nilikuwa nikiyasikia tu toka kwa wale wa rika langu bila kujali jinsia. Hakuna anayeweza kubisha kwamba wanapokutana watu wa rika moja si muda wote huwa wanakuwa serious, kuna wakati hali hubadilika na maneno mbadala hutumika ili kuchagiza story. (siwezi yataja hapa). Baada ya utangulizi huo,napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa mke wa Ngugi wa Thiong'o anayejulikana kama Nyeri wa Ngugi. Bila shaka unakumbuka mkasa uliowapata yeye na mme wake walipoitembelea Kenya mwaka 2005.Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari, mama huyu mbele ya kadamnasi iliyokuwa imekusanyika katika ukumbi wa Silver Centre hapa New York University alibainisha ukweli na kwa kuyatumia maneno halisi kwamba walipovamiwa na majambazi licha ya kuporwa pia walitenganishwa vyumba na hatimaye wakamuingilia kwa nguvu (kumbaka). Akiendelea kufafanua anasema alikuwa anahofia sana kuambukizwa ukimwi na si vinginevyo.Lakini kwa taratibu za wanawake wa Kenya na Afrika kwa ujumla ni nadra sana kwa mtu aliyeolewa kusema amebakwa. Yawezekana ni kwa kuogopa talaka au aibu (mimi sijui). Sasa kutokana na hii tabia ndio maana ninadiriki kutoa shukrani kwa mama huyu aliye na umri zaidi ya mama yangu kwa kuwa muwazi na kuyatamka hadharani maswahibu yaliyompata. Hii ni changamoto kwa wanawake hasa walio kwenye ndoa ya kwamba "koleo ni lazima waliite koleo"

Monday, January 22, 2007

Upi muziki wa Tanzania?

Wahenga walinena "kazi na dawa".Ndivyo inavyojidhihirisha katika picha ambapo waafrika mbalimbali waliamua kuifurahia ladha ya taarabu wakati wa sherehe za kuanza muhula wa pili wa masomo hapa NYU. Sipo pichani,ila kabla ya hapo niliwapa shule kidogo namna ya kuicheza na hayo ndo matokeo yake.

Miongoni mwa maswali magumu nilowahi kuulizwa ni hili la kuhusu muziki wa Tanzania.Kwa sababu ilikuwa ni mkusanyiko wa Waafrika mbalimbali na wengi wao walikuwa kutoka Afrika magharib,msema chochote hakuchelewa kuniita na mara baada ya kunitambuza aliniuliza ni upi muziki ambao ni kielelezo cha Tanzania kiasi kwamba ukiusikia tu unajua huu ni kutoka Tanzania? Palikuwa hapatoshi lakini kwa vile nilikuwa na CD za taarabu ikabidi nimwambie ni "taarabu" ili kuepuka aibu ya kuiangusha nchi yangu miongoni mwa macho ya wageni wengine. Basi kutoka kwenye hiyo CD ya East Africa Melody kilipigwa kibao cha "viumbe wazito" na nika-demonstrate namna ya kuicheza taarabu kabla ya hadhira kunyanyuka na kuniunga mkono. Baada ya hizo dondoo chache narudi kwenye mada kuu kwamba upi hasa ndo muziki wa Tanzania? Nashindwa na sijui sawasawa kati ya mduara,taarabu,dansi,bongo flava, n.k ni upi ndo kielelezo cha muziki wa Tanzania. Dunia kwa hivi sasa imekuwa kijiji kimoja na kwa maana hiyo waweza kutumia lugha yoyote ile lakini bado uka-maintain muziki wa asili yako.Mfano halisi ni kundi la Mandinka toka Afrika magharib wana wimbo wao moja wenye maneno mengi ya kiswahili lakini bado ukiusikia unajua kabisa ni kutoka Afrika ya magharibi.Kwa anayejua anisaidie kunijuvya ni upi hasa ndo muziki wa Tanzania?




Wababe wa kivita.

Tukiwa mbele ya sanamu la mashujaa sambamba na "double M" mjini Washington DC.

Katika hali ya kawaida vita si lelemama na wala si suala la kuombea.Ukilinganisha kati ya faida na hasara za vita, haiyumkini hasara zitachukua asilimia kubwa kuliko faida.Pamoja na hayo kuna vita visivyoepukika na vipo vita vya kuepukika.Si lengo langu kujadili aina za vita. Kama picha inavyojieleza, hiyo ni sehemu maalum kwa ajili ya kutunza kumbukumbu ya mashujaa walioshiriki vita vya Vietnam.Nchi ya Marekani inawaenzi kwa namna ya kipekee mashujaa wao al-maarufu kama"wababe wa kivita".Nini somo kwa nchi yetu ambayo miaka ya 1978 ilijikuta katika vita dhidi ya nduli Idd Amin Dada? Binafsi naona umefika wakati sasa kwa serikali ya Tanzania kuwaenzi wapiganaji wetu (wababe wa kivita chini ya amiri jeshi mkuu hayati Mwl. Nyerere) kwa namna walivyojitoa muhanga na hatimaye kuinusuru sehemu ya ardhi ya nchi yetu iliyotaka kuporwa na Nduli. Tuwape heshima stahili wote waliopoteza maisha wakati wa vita na pia washiriki wote ambao bado wapo hai. Mathalani serikali inaweza ikawaenzi kwa kutoa 50% ya ada kwa watoto wa mashujaa walau katika shule za sekondari. Nategemea maoni mujarabu kutoka kwenu.

Thursday, January 18, 2007

Kandanda ni kipaji na elimu pia.

Pichani Mwl. Merchedes Method (katikati) aliye chuo kikuu cha Wisconsin akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa kocha wa chuo (hayupo pichani) wakati wa mapumziko. Katika mechi hiyo Wisc. walishinda 2-0 huku yeye akiwa kapachika kimiani bao moja.
Wakati dunia hivi sasa inashuhudia maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia katika kila nyanja, soka la Tanzania limeendelea kutawaliwa na vibweka vinavyoashiria imani kali za kishirikina kama inavyokuwa wakati wa mpambano wa vigogo vya soka nchini Simba na Yanga.Umefika wakati sasa kuachana na imani hizo na kuwekeza katika rasilimali watu ili kuinua kiwango cha kabumbu la bongo.Tanzania imejaliwa vipaji vingi vya wachezaji. Mojawapo ya vipaji hivyo ni kijana Merchedes Method (double M) aliye katika chuo kikuu cha Wisconsin nchini Marekani. Licha ya kufundisha kiswahili chuoni hapo,pia amejijengea umaarufu mkubwa katika fani ya mpira wa miguu maarufu kama futibo.Amekuwa gumzo chuoni hapo kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira,kupangua misitu ya mabeki kwa chenga za maudhi na pia kwa mashuti yake mazito.Habari njema kwa Tanzania kwa ujumla ni kwamba kijana huyo pia anahudhuria mafunzo ya ukocha chuoni hapo.Tunamuomba akimaliza muda wake arejee nchini na kuboresha mchezo wa mpira wa miguu.

Monday, January 15, 2007

Dhana ya sadaka.

Muongozo wa dini ya kiislam.
Sadaka katika lugha rahisi ni kitu chochote kinachotolewa na mwenyenacho ili kumsaidia asiyekuwa nacho. Kiundani, mtu yoyote anaweza kutoa sadaka bila kujali kama ni tajiri au masikini. Inasemekana sadaka ya masikini ni bora zaidi kuliko sadaka ya tajiri.Sadaka inaweza ikawa chakula,mavazi,fedha n.k. Dini zote zimeweka wazi kwamba sadaka ni siri kiasi kwamba kama umeitoa kwa mkono wa kulia basi hata ule wa kushoto usijue kuwa mkono wa kulia umetoa nini.Kimsingi sadaka sio jambo la kutangaza kwa maana ya kwamba unapoitoa,unakuwa unamtolea Mungu naye anakuona.Kama utaitoa sadaka kwa minajili ya kujipatia umaarufu/ufahari ama hakika haiwezi pata baraka toka kwa Mungu.Maoni yangu ni kwamba sadaka zitolewe kama dini zetu zinavyoelekeza.

Friday, January 12, 2007

Hivi kweli taifa linakabiliwa na uhaba wa walimu?

(Pichani Mwl.Ngugi alipolitembelea darasa langu la kiswahili.Umefika wakati kwa serikali ya Tanzania kuwathamini walimu kwani walimu ni funguo za fani anuwai.)

Kama ambavyo haijulikani ni kipi kilitangulia kati ya kuku na yai,hali kadhalika na mimi sijui ni kipi kinatangulia kati ya elimu na maendeleo.Ninachoweza kusema, elimu ni chachu (catalyst) ya maendeleo.Elimu ni neno moja ambalo linabeba maana pana na inayojitosheleza.Wanazuoni mbalimbali walitoa nadharia zao juu ya neno hili.Mathalani Aristoto analifafanua neno elimu kama kitendo cha mtu kuweza kuyafahamu yale asiyokuwa akiyafahamu hapo awali.Aristoto anaendelea kuielezea elimu kama ni kitu ambacho kipo siku zote tangu siku mwanadamu anapozaliwa hadi siku ya kufa.Kimsingi elimu ni chachu ya maendeleo kwa jamii yoyote hapa duniani.
Ili kuweza kutoa elimu bora vinahitajika vitu vikuu vitatu; mosi - miundo mbinu kama vile vyumba vya madarasa, pili -walimu bora na tatu-vitendea kazi kwa ujumla wake.Kwa ujumla tatizo kubwa katika huo utatu ni ukosefu kama si upungufu wa walimu.Hili limekuwa tatizo lisilopatiwa ufumbuzi wa kudumu hapa nchini.Siyo shule za msingi wala sekondari au vyuo vikuu,muziki ni ule ule tu; yaani uhaba kama si upungufu wa walimu.
Ukiondoa miji mikubwa kama vile Dar es Salaam,Mwanza na Arusha na pengine katika kila makao makuu ya mikoa na wilaya ni mifano michache ya sehemu ambazo zinajitosheleza.Kwa upande mwingine hali ni mbaya katika maeneo mengine hususani vijijini. Mathalani shule za sekondari zimefunguliwa na zinaendelea kufunguliwa katika kila kata huku zikiwa hazina walimu wa kutosha na lau kama wapo basi ni chini ya idadi na viwango vinayotakiwa.
Kwa ujumla idadi ya walimu wanaohitimu mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya stashahada na shahada ni ya kuridhisha na kama wote wakipatiwa mazingira mazuri ya kufanya kazi katika maeneo mbalimbali yenye upungufu hakika tatizo la upungufu wa walimu linaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Changamoto kwa wizara ya elimu na mafunzo kwa kushirikiana na wizara za sayansi teknolojia na elimu ya juu na ile inayoshughulikia masuala ya ajira waliangalie suala hili kwa mapana yake ili Tanzania iachane na wimbo wa ukosefu wa walimu katika shule za sekondari zinazomilikiwa na serikali pamoja na zile za wazazi kwa kutoa ajira kwa wahitimu wote wa fani hiyo ikiwa ni sambamba na maslahi mazuri kama zilivyo sekta nyingine hapa nchini. "Ualimu ni kazi bwana na wala sio wito".

Tuzithamini bidhaa za ndani.

(Pichani; Bidhaa za kigeni ambazo kimsingi tunakula ili tushibe. Mara nyingi vyakula hivi huwa havina ladha nzuri na asilia.)

Binadamu tunatofautiana kwa silka na hulka. Kila mtu ana tabia zake ambazo haiyumkini zaweza kuwa nzuri au mbaya pia. Binafsi naweza sema umaarufu ni moja ya sifa kubwa inayotafutwa kwa nguvu zote na asilia kubwa ya binadamu. Kuna haja gani ya kwenda kulinunua chenza toka Afrika ya Kusini lenye ubora sawa na lile linalotoka Muheza kwa bei ya juu? Hainingii akilini na ndio maana naona kama huo ni utafutaji tu wa umaarufu.
Kwa bidhaa za mashambani Tanzania tumejaliwa (endowed) aina mbalimbali za vyakula vilivyo na ubora wa kutosha.Mathalani kuna machungwa yanaozea mitini huko Muheza,kuna milima kama si vifusi vya mananasi pale Chalinze,kuna ndizi nyingi huko Tukuyu,Mlimba na Bukoba.Viazi pia vipo vya kutosha huko Njombe na Morogoro.Nyanya zinapatikana kwa wingi Iringa na Morogoro.Hiyo ni mifano michache tu.Pamoja na uwingi wa bidhaa bora toka ndani ya nchi, haiyumkini bado kuna hizi zinazoitwa "Shopping centres" mijini zenye kuuza bidhaa za kigeni za mashambani kama vile matunda kutoka nchini Afrika ya Kusini tena kwa bei ya juu. Umefika wakati sasa kwa walaji kubadilika na kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwetu kwamba kila kinachotoka ng'ambo ni bora.Sambamba na hilo kuna haja ya kuboresha mazingira na kukuza soko la bidhaa za ndani kwa minajili ya kuwanusuru wakulima na wazalishaji wa ndani na pia kukuza pato la taifa.Kwa ufupi linahitajika soko madhubuti na mipango endelevu kwa ajili ya bidhaa za ndani.Tusipokuwa makini kuna siku maduka haya makubwa yatatuuzia chapati zilizookwa Afrika ya Kusini na Uarabuni.