Saturday, February 3, 2007

Tutaamka kikieleweka!!!

Ni kupumzika tu muda wowote na mahala popote. Picha kutoka darhotwire.

Ni wimbo ambao unatia fora karibu ulimwenguni kote. Wimbo wenyewe si mwingine bali ni ule uliopo kwenye albamu ya siku nyingi ya uchumi unaokwenda kwa jina la ajira. Kwa nchi zilizoendelea (za dunia ya kwanza) wimbo huu si maarufu sana. Kwa upande wa nchi zinazoendelea, wimbo huu ama hakika unatikisa vilivyo kila uchao. Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea inajitoa muhanga kwa kufanya kila linalowezekana kupunguza idadi ya wananchi hususani vijana wanaoimba kibao hiki japo kimepitwa na wakati ikizingatiwa ni karibu miaka 45 tokea nchi yetu ipate uhuru. Katika kufanikisha uwezeshaji kwa wananchi, serikali ya awamu ya nne chini ya Mh. Raisi J.Kikwete imeisha toa shilingi bilioni 1 kwa kila mkoa. Kwa ujumla ni mwanzo mzuri kama kutakuwa na usimamizi mzuri na masharti nafuu ili kuwawezesha walengwa haswaa kupatiwa mkopo huo. Vile vile ni wakati mzuri pia kwa benki zetu na asasi binafsi kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa wananchi ili kuchagiza mchakato mzima wa kuwawezesha wananchi kujiajiri wenyewe. Kama haya yote yatafanyika na mazingira mazuri yataandaliwa bila shaka hata waliolala wataamka. Namalizia kwa kusema "kama wao wameweza wana nini na sisi tushindwe tuna nini?"

2 comments:

Anonymous said...

Hii ndiyo Danganyika bwana mdogo!!!

Simon Kitururu said...

Kama wao wanaweza naamini na sisi tunaweza